
KKKT Dayosisi ya Kusini iliandaa semina ya wachungaji na wainjilisti wa Jimbo la Njombe, iliyofanyika katika Usharika wa Matiganjola kuanzia tarehe 28–30 Aprili 2026. Lengo kuu lilikuwa kuwaleta pamoja watumishi wa Mungu ili kukumbushana wajibu wetu na kuimarisha mshikamano wa huduma.
UFUNGUZI WA SEMINA
Semina ilifunguliwa rasmi tarehe 29/4/2026 asubuhi na Mkuu wa Jimbo, Mchungaji Nuru Kahwili, akisimamia maandiko ya Yakobo 5:15–18. Alisisitiza kuomba kwa bidii, kufanya kazi kwa moyo, na kuwa na nidhamu ya kazi, akikazia kwamba lolote tufanyalo tulifanye kwa ajili ya Bwana, si kwa wanadamu.

SOMO LA KWANZA: PANUA HEMA
Liliwasilishwa na Baba Askofu wa KKKT Dayosisi ya Kusini, Mchungaji Dr. George Mark Fihavango, akisimamia maandiko ya Isaya 54:2–3.
Alisisitiza kupanua makanisa kwa sababu ya ongezeko la watu, kupanua maono kuanzia ngazi ya jumuiya, kuondoa vizuizi katika huduma (hofu, mazoea, mifumo mibovu, uvivu na ubinafsi), na kukaza vigingi kwa mafundisho ya kweli.
Aidha, alifafanua agenda kubwa za Dayosisi: injili na mpeleka injili, mfumo wa bima, mfuko wa maendeleo ya Dayosisi, mpango wa kuwaaga wachungaji na wainjilisti wastaafu, pamoja na masuala ya uchumi na kujitegemea kwa washarika na watumishi. Pia alisisitiza uhusiano binafsi na Mungu na maisha ya kifamilia ya mtumishi (Mithali 13:22; 1 Timotheo 5:8).

SOMO LA PILI: ITIFAKI
Liliwasilishwa na Mwalimu Petro Kilima, Katibu Mkuu Msaidizi wa Dayosisi ya Kusini.
Alifundisha umuhimu wa itifaki katika utumishi wa kanisa, akieleza kuwa ni msingi wa nidhamu, heshima na mshikamano wa huduma, na inalinda taswira ya kanisa mbele ya jamii.

SOMO LA TATU: MATOLEO NA SADAKA
Liliwasilishwa na Mtunza Hazina wa Dayosisi ya Kusini, Yohana Ndelele.
Alitoa ufafanuzi juu ya aina mbalimbali za matoleo na sadaka, akisisitiza kuwa ni ibada ya kiroho na ishara ya shukrani kwa Mungu, huku pia zikisaidia kuimarisha huduma, ustawi wa watumishi na maendeleo ya kanisa.
SOMO LA NNE: MAONO YA MTUMISHI & UENDELEVU WA KAZI YA MUNGU
Liliwasilishwa na Msaidizi wa Askofu, Mchungaji Dr. Johnson Gudaga.
Alifundisha maana ya maono na kueleza kuwa ili kufanikisha maono lazima kuwe na: maono – lengo – mkakati – kazi halisi. Pia alisisitiza usimamizi wa rasilimali (watu, muda na fedha).
Kupitia somo hili, alieleza maono ya Dayosisi ya Kusini ya kujenga Lutheran Mall kwa ajili ya maendeleo ya Dayosisi, ili kuimarisha uchumi na maslahi ya watumishi bila kutegemea sadaka pekee. Alifafanua lengo la Sadaka ya Maendeleo ya Dayosisi, na washiriki waliguswa kiasi cha kuanzisha harambee ndogo, ambapo jumla ya fedha taslimu zilizopatikana zilikuwa Tsh. 2,667,000/=.

HITIMISHO
Semina hii imekuwa baraka kubwa kwa wachungaji na wainjilisti wa Jimbo la Njombe. Kupitia masomo haya, tumekumbushwa kuomba kwa bidii, kufanya kazi kwa moyo, kuimarisha maono, kushiriki matoleo kwa uwajibikaji, na kusimamia rasilimali kwa ufanisi.
Kwa pamoja tunakiri kwamba semina hii imeweka msingi wa mshikamano, nidhamu na uwajibikaji katika utumishi, na ni mwaliko wa kuendeleza yale tuliyojifunza kwa vitendo katika makanisa, jumuiya na familia zetu.