
Seminari ya Kilutheri Kidugala.
NDIYE MBARIKIWA AJAYE KWA JINA LA BWANA
Zaburi 98:1-4, Mathayo 21:1-11 Zekaria 9:8-12.
Wapendwa katika Bwana, karibuni kwa Bible study ya masomo ya jumapili ya tarehe 29/03/2026, Jumapili ya Mitende yenye wazo la juma linalosema, _Ndiye Mbarikiwa ajaye kwa Jina la Bwana._ Tutaongozwa na masomo ya Biblia kutoka Zaburi ya 98:1-4, Mathayo 21:1-11 na Zekaria 9:8-12 pamoja na wimb0 wa siku hiyo, na.1 TMW.* Pamoja na mafafanuzi kwa sehemu ya masomo hayo naambatanisha na maswali ya mjadala mwishoni, karibuni;
Somo la kwanza: Zaburi 98:1-4
Kimsingi kitabu cha zaburi ni kitabu cha nyimbo tena zinazoambatana na ala za muziki kama tunavyosoma kwa mfano Zaburi 150:1-6. Nawapongeza watunzi mbalimbali wanaojitahidi kutengeneza sauti zake ili watu waimbe kwa kuwa ndivyo ilivyokusudiwa.
Zipo namna mbili za kuanisha zaburi. Njia mojawapo ni kugawanya zaburi katika makundi matano ambayo maudhui yake yanaelekeana na vitabu vitano vya sheria. Katika fungu la kwanza ambalo linaitwa kitabu cha kwanza maudhui yake yanafanana na yale ya kitabu cha Mwanzo (Zaburi 1-41). Kitabu cha pili (Zaburi 42-72) kina maudhui yanayofanana na kitabu cha Kutoka. Kitabu cha tatu (Zaburi 73-89) kina maudhui yanayoelekeana na kitabu cha Mambo ya Walawi, kitabu cha nne (Zaburi 90-106) ambapo na Zaburi ya 98 inaangukia, kina maudhui yanayoelekeana na Kitabu vha Hesabu yaani safari ya wana wa Israeli. Hatimaye, kitabu cha tano (Zaburi 107-150) ambazo ni zaburi za sifa na shukurani kina maudhui yanayokaribia yale ya Kumbukumbu la Torati.
Njia ya pili ni kugawanya zaburi kwa kuangalia yaliyomo yaani zaburi za sifa na shukurani, zaburi za maombolezo, zaburi za kukwea Sayuni, Zaburi za kumwomba Mungu aingilie kati na kulipiza kisasi au zaburi za kumwombea mfalme. Hapo Zaburi 98 inaangukia kwenye zaburi za sifa na shukurani.
Zaburi ya 98 ni wimbo wa shukrani na sifa kwa Mungu! Inatukumbusha kuimba wimbo mpya kwa Bwana kwa sababu ya matendo yake makubwa. Mwimba zaburi anaeleza sababu za kumwimbia Mungu wimbo mpya. Yeye ndiye aliyetuumba, ndiye aliyetukomboa naye anatawala dunia yote. Mwaliko wa kumsifu Mungu ni kwa watu wote na viumbe vyote duniani.
Zaburi hii inatujia wakati huu Yesu anapouendea msalaba ambao ndio msingi wa wokovu wetu! Neno la msalaba kwa wanaopotea ni upuzi bali kwetu sisi ni nguvu iletayo wokovu (1Kor. 1:18-20). Kwa kupigwa kwake sisi tumepona!!!
Wimbo mpya maana yake tusimsifu Mungu kwa mazoea au kwa kutimiza tu taratibu za ibada. Sifa na nyimbo za kumwelekea Mungu zinaanza moyoni mwa mtu! Tumsifu Mungu wetu kwa akili na kwa moyo.
Somo la pili: Mathayo 21:1-11
Katika somo hili la pili tunasoma kuwa Yesu pamoja na wanafunzi wake wanapokaribia Yerusalemu aliwatuma wanafunzi wake wawili waende kijiji kilichokuwa kinawakabili ambako wangemwona punda na mtoto wa punda wawafungue. Ndivyo walivyofanya wakatandika nguo juu yao na Yesu akapanda juu yake. Zekaria anaonesha na kusisitiza wazi kuwa mfalme ajaye Sayuni, amepanda punda na kusisitiza, naam, mtoto wa punda kama kielelezo cha amani, unyenyekevu na upole wa Yesu. Yesu anaingia Yerusalemu kama mfalme wa amani, mpole na mnyenyekevu! Laiti kama tungeelewa aina ya uongozi ambao Baba Askofu anasisitiza _KAIZEN,_ nadhani taasisi zetu na dayosisi yetu ingekuwa mahali ambapo injili inahubiriwa na sakramenti inatolewa kwa usahihi. Mara ngapi tumejisifu na kuona kuwa mafanikio ya kanisa yametokana na nguvu zetu na akili zetu na kusahau nafasi ya Mungu maishani mwetu? Ni mara ngapi tumewapa wengine fursa ya kutushauri ili kuboresha utendaji wetu au tunajiona tumefika? Yesu anatupa kielelezo cha maisha ya kikristo na uongozi bora; amani, upole na unyenyekevu.
Somo la tatu: Zekaria 9:8-12
Zekaria 9:8-12 ni ujumbe wa matumaini ya ukombozi. Kama tulivyosoma Zaburi ya 98:1-4, Zekaria 9:8-12 ni mwaliko wa kufurahi na kushanglia ujio wa mwenye haki, mkombozi na mnyenyekevu. Kupanda punda ilikuwa ishara ya amani na unyenyekevu. Aidha, kupanda punda tena mtoto wa punda ni kuonesha kuwa alikuja kwa watu wa kawaida kabisa tena bila majivuno. Aidha, Yesu pia aliwagundisha wanafunzi wake kwa vielelezo kuwa ukubwa kikristo ni kuwatumikia watu na siyo kuwatumikisha. Anayoa kielelezo hicho kwa mfano, anapowatawadha wanafunzi wake miguu na kuwahimiza kuwa hivyo ndivyo wanavyopaswa kutendeana. Tunaweza kujitathmini sisi tulio viongozi leo ni kwa kiasi gani bado tunayo nia ya Yesu au tumepotea kiasi gani? Je, tunawafikia watu wa kawaida au tunawafikia wenye pesa tu? Tunawasogeza watu kwa Mungu au tunawakimbiza mbali na Mfalme mwokozi wao? Utumishi wetu unawaletea watu matumaini ya ukombozi au unawavunja moyo?
Swali la kujadili:
Yesu akiwa njiani kuelekea Yerusalemu, aliendelea na huduma yake kama kawaida. Aidha, anapoukaribia msalaba, alitengeneza mazingira ya watu kumshangilia mkombozi wao. Hata mafarisayo walipomtaka awakanye wanafunzi wake wasimshangilie alisisitiza kuwa kama wangenyamaza angeinua mawe yamsifu anapouendea msalaba!
Sisi leo tumekaza kuwanyamazisha washarika wasimsifu Mungu, wasiimbe Haleluya (Msifuni Bwana) wala utukufu kwa Mungu kwa jina la Kwaresma. Najiuliza sisi tuko upande gani; wa Yesu aliyewataka wamshangilie anapouendea msalaba au wa mafarisayo wanaowanyamazisha watu wasimshangilie wala kumsifu Yesu anapouendea msalaba ambao ndio sababu ya ukombozi wao? Kwa kawaida nafsi au akili ya mtu huwa inatengeneza au kutaka kitu mbadala wa kinachoondolewa; sasa najiuliza kwa sauti ya chini,
Tunapowanyamazisha hawa watu wa Mungu wasimsifu mkombozi wao kwa jina la Kwaresma, tunataka wamsifu nani badala yake? Tukisema UTUKUFU tusiimbe ni nini tunataka hawa walio wadogo waimbe badala yake? Msalaba ni alama ya ushindi na ndiyo sababu ya mashangilio yetu. Kwa nini tunyamaze na kwa nini tuwanyamazishe wanaoona sababu ya kushangilia ushindi wa msalaba?
Hebu tutafakari pamoja maana ya wimbo namba 22, Tenzi za Rohoni, unaoimbwa, _Kale nilitembea_
_
1. Kale nilitembea, nikilemewa dhambi, nilikosa msaada, kuniponya mateso.
Usifiwe msalaba
Lisifiwe kaburi
linalozidi yote
Asifiwe Mwokozi
2. Hata nilipofika, mahali pa msalaba palinifaa sana, sitasahau kamwe.
3. Hicho ndicho chanzo cha kufurahi kwangu. Hapo ndipo mzigo uliponituliwa.
4. Mahali pa msalaba kinatolewa cheti cha kuingia mbinguni kisicho cha kanisa.
5. Yule bwana mjinga likwenda bila cheti kitunai kwingia kama walio nacho.
6. Lipofika langoni akaulizwa cheti cha kumwonyesha Bwana akakutwa hanacho.
7. Lituhuzunishalo ni ninyi msio nacho kuwa kama mjinga kwa siku ya arusi!
8. Ubavuni mwa Yesu mlitokea damu chemchemi ya uzima itakasayo roho.
9. Jitahidi wingie damuni mwa Mwokozi, utafutiwa dhambi toka rohoni mwako_ .
Mungu atusaidie ili utumishi wetu uwe kimbilio la watu wamwone Yesu mfalme wa amani kwa njia yetu, Amen.