Mchg. Dk. Johnson Gudaga
Msaidizi wa Askofu wa ELCT – SD
OKULI – MACHO YANGU YANAMTAZAMA BWANA
Somo la Kwanza: Zaburi 147:14–20
Somo la Pili: Ufunuo 4:11
Somo la Mahubiri: Ayubu 12:7–10
- UTANGULIZI
Watu wa Mungu Wapenzi, Shalom.
Tunakaribisha sana kushiriki kwa roho ya umoja na upendo katika Masomo ya Biblia ya leo, tunapojitayarisha kwa Ibada ya Jumapili ya Nne kabla ya Pasaka. Tunakutana mtandaoni si kwa ajili ya maandalizi ya mahubiri tu, bali kwa lengo la kujengana, kushirikiana vipawa, kutiana nguvu kiroho, na kutafakari pamoja Neno la Mungu litakalohubiriwa madhabahuni Jumapili ijayo.
Mchakato huu unatukumbusha kwamba huduma ya Neno si wajibu wa mtu mmoja, bali ni wito wa pamoja. Tunapojadiliana hili kabla ya Jumapili, tunafanya mambo matatu muhimu:
- Tunajenga umoja kati ya wahudumu wa Neno.
- Tunachimba kirefu katika misingi ya kiteolojia ya maandiko.
- Tunajitayarisha si kuhubiri tu, bali kuishi kile tutakachohubiri.
Katika kipindi hiki cha Kwaresma, chini ya mada kuu ”Okuli – Macho Yangu Yamemwona Bwana”, tunakaribisha kutazama kwa makini zaidi kwa Mungu. Tunamtazama si kama Mwokozi tu, bali pia kama Muumba, Mmiliki, na Mtegemezi wa viumbe vyote. Hapa ndipo mada ya wiki hii inapopata umuhimu wake: ”Mazingira ni Uhai – Tuyatunze.” Suala la uangalizi wa mazingira si jambo la busara tu, ni pia jambo la imani. Kulingana na Kalenda ya Masomo ya Biblia ya ELCT, kwa Jumapili ya Nne kabla ya Pasaka (Okuli – Macho Yangu Yanamtazama Bwana), kanisa limepanga masomo matatu yasomwe katika ibada ya Jumapili kama ifuatavyo:
SOMO LA KWANZA: ZABURI 147:14–20
Miongoni mwa mambo mengine, mistari hii (14-20) inatufunulia kwamba amani inatoka kwa Mungu na kwamba Mungu ndiye anayedumisha amani na usalama wa watu wake, hivyo kudumisha mamlaka yake (mst. 14). Inathibitisha kwamba Mungu anasimamia hali ya hewa na matukio ya asili kwa utaratibu na hekima (mist. 16-17). Zaidi ya hayo, mwandishi wa zaburi anaonyesha kwamba kufuata sheria za Mungu kunaleta mwongozo na amani kwa watu wake. Na kwamba baraka za kiroho zinatokana na kufuata amri zake, si juhudi za mtu binafsi peke yake (mst. 18).
Kwa maana hii, tunaona wazi hapa kwamba amani, chakula, na ustawi wa kijamii vimeunganishwa na utaratibu wa Mungu katika asili. Amani si suala la kisiasa tu; ni matokeo ya utaratibu sahihi wa uumbaji wa Mungu. Chakula si matokeo ya juhudi za binadamu peke yake; ni baraka inayotiririka kupitia ardhi, mvua, misimu, na uzalishaji ambao Mungu anauwezesha. Mazingira yanapoharibiwa, ustawi wa kijamii unaporomoka.
Kwa mfano; Ukataji miti husababisha kupungua kwa mvua na vyanzo vya maji. Ukame husababisha njaa. Njaa husababisha migogoro ya kijamii, migogoro ya rasilimali, na hata kuvunjika kwa mshikamano wa kijamii. Hapa tunaona wazi kwamba theolojia ya uumbaji ina uhusiano wa moja kwa moja na haki za kijamii. Uharibifu wa mazingira mara nyingi huwadhuru zaidi maskini, ambao wanategemea ardhi na maji kwa maisha yao ya kila siku.
Katika mazingira yetu, ni jambo la faraja na tumaini kuona juhudi zinazofanyika ndani ya kanisa letu. Hapa mnaweza kujiunga nami kumhongeza wenzetu katika Chuo Kikuu cha Utheolojia cha Kilutheri cha Kidugala, hasa Chuo cha Biblia, kwa kukuza na kuendeleza vitendoni Theolojia ya Kijani inayotunza na kuhifadhi mazingira. Hii si theolojia ya kinadharia tu, bali ni theolojia inayoshuka ardhini, kupanda miti, kulinda vyanzo vya maji, na kufundisha vizazi vipya kuwa na wajibu kwa uumbaji wa Mungu. Nadhani si kosa kutaja kwa nia njema Mkuu wa Chuo, Mchg. Mexon Mng’ong’o, kwa kazi kubwa ya kusema wazi kuhusu ajenda ya utunzaji wa mazingira katika mikutano mbalimbali, hata katika hali zisizo za kawaida kama majanga. Pale tunaona ujasiri wa kinabii: kuunganisha Neno la Mungu na changamoto halisi za jamii. Kwa ujumla, tunakumbushwa kama wachungaji kutazama kwa kina Neno na kulitafsiri katika maisha halisi ya watu. Kwa kufanya hivyo, tunaonyesha kwamba: Utunzaji wa mazingira ni sehemu ya wito wa kichungaji, ni sehemu ya huduma ya upatanisho kati ya Mungu, mwanadamu, na viumbe na ni sehemu ya kuishi Injili katika ulimwengu halisi. Ninapokamilisha sehemu hii ya kwanza, ningependa kuuliza swali hili: Ikiwa Mungu anaendelea kutegemeza viumbe vyake, je, sisi kama kanisa tunashirikiana naye au tunapingana naye kwa matendo yetu?
SOMO LA PILI: UFUNUO 4:11
Sote tunajua kwamba Kitabu cha Ufunuo kiliandikwa na Mtume Yohana (Yohana wa Patmo) wakati wa mateso ya Wakristo wa mwanzo chini ya Dola la Kirumi, karibu mwisho wa karne ya kwanza (kati ya 95–96 BK). Yohana alirekodi maono haya kutoka kisiwa cha Patmo, ambapo alikuwa amefungwa kwa ajili ya imani yake. Ni jambo linaloeleweka kwamba Wakristo wa mwanzo walipata dhuluma, mateso, na shinikizo la kifamilia na kijamii. Kwa hivyo kitabu cha Ufunuo kilikuwa sauti ya kutia moyo, kuimarisha imani, na kuonyesha kwamba Mungu ana mamlaka juu ya historia yote na matukio ya ulimwengu. Kimsingi, kitabu hiki ni kitabu cha kutia moyo, kinachoonyesha ushindi wa mwisho wa Mungu juu ya uovu, na kuwatia moyo watu kuishi kwa uaminifu.
Sura ya 4 inaanza na Yohana kuona mlango uliofunguliwa mbinguni na kiti cha enzi cha Mungu (Ufunuo 4:1–2). Hii ni sehemu ya maono ya utukufu wa Mungu, inayoonyesha mamlaka yake juu ya ulimwengu wote. Yohana amezungukwa na malaika, viumbe hai, na wazee wanaomsifu Mungu mchana kutwa. Maono haya hayana uhusiano na ulimwengu wa kawaida; ni mtazamo wa kiroho unaofundisha: Mungu ana mamlaka kamili, Kila kiumbe cha uumbaji kinamshukuru Mungu, na kwamba Utukufu wa Mungu unastahili sifa zisizo na mwisho. Mstari wa 11 (somo la leo) unafafanua wazi kwamba kila kitu kiliumbwa kwa mapenzi ya Mungu, na uhai na uzuri wa vyote ni zawadi kutoka kwake. Kwa Wakristo, maono haya ni chanzo cha tumaini, amani, na sifa; Mungu anasimamia maisha yetu, historia, na viumbe vyote katika hekima yake. Kabla ya kusifiwa kwa ukombozi, Mungu anasifiwa kwa uumbaji. Hii inaonyesha kwamba uumbaji una thamani ya kiroho. Kwa kweli, ibada ya kweli haiwezi kutenganishwa na uumbaji. Nimejifunza kwamba, Ikiwa kanisa linaimba sifa Jumapili lakini linawacha takataka zikiwa zimesambaa, kuna kutokuungana kati ya ibada na maisha. Ninapotafakari somo hili, nimetambua kwamba ibada si tukio la saa moja. Ni njia ya maisha ambapo kanisa linaweza kupanda miti kama ishara ya toba ya Kwaresma, kukuza matumizi endelevu ya ardhi, na kufundisha wajibu wa mazingira. Hapa najiuliza swali hili muhimu: Je, kanisa linalopuuza uharibifu wa mazingira linaweza kusema linatimiza kikamili wito wake wa ibada?
SOMO LA TATU: AYUBU 12:7–10
Kitabu cha Ayubu ni mojawapo ya vitabu vya hekima vya Biblia, vinavyoshughulikia maswali magumu ya maisha: mateso, haki, hekima, na uhusiano wa mwanadamu na Mungu. Ayubu, katika mateso makubwa na kushughulika na hoja za rafiki zake, anawakumbusha wasikilizaji wake na wasomaji kwamba hekima ya Mungu si katika maneno tu, bali pia katika viumbe vyote. Hapa mwandishi anatumia mifano kutoka kwa viumbe (wanyama, ndege, ardhi, samaki) kuelezea hekima ya Mungu. Anafundisha kwamba hekima inaweza kupatikana kwa kuchunguza uhai na viumbe vya Mungu. Mistari hii inafunua mafunzo ya kiroho, hekima ya Mungu, na thamani ya uhai kupitia viumbe. Hii inafundisha kwamba kuchunguza uhai wa kila kiumbe kunaweza kufunua siri za Mungu.
Ayubu alikuwa mtu aliyeishi katika ulimwengu wa kale, ambapo watu walithamini hekima, utajiri, na heshima ya kijamii. Katika kipindi hiki, mateso mara nyingi yalionwa kama adhabu ya dhambi. Rafiki za Ayubu walijaribu kumshawishi kwamba mateso yake yalikuwa kwa sababu ya dhambi, lakini Ayubu alipinga hoja hiyo kwa kusema kwamba hekima na nguvu za Mungu ni kubwa kuliko mawazo ya binadamu.
Tukiangalia mistari ya 7 na 8, mistari 7–8 tunaona kwamba Hekima ya Mungu iko katika viumbe. Kwamba kila kiumbe kinatufundisha sifa za Mungu: Kwa mfano; Nyuki na wanyama wengine wanatufundisha kuhusu bidii, ushirikiano, na uvumilivu. Mimea na miti inatufundisha kuhusu uvumilivu, mafanikio, na kutegemea baraka za asili. Samaki na viumbe vya baharini vinatuelekezea kwenye utaratibu wa uhai na utajiri wa asili. Kimsingi, mistari hii inatufundisha kwamba kila kiumbe ni mwongozo wa kiroho, na kutazama viumbe ni njia ya kupata hekima ya Mungu.
Tukiendelea kwenye mstari wa 9, Ayubu anathibitisha kwamba Mungu ndiye Muumba wa viumbe vyote na kwamba hakuna kinachotokea bila idhini yake. Mamlaka ya Mungu ni kamili na inaonekana wazi katika utaratibu wa viumbe. Hapa Ayubu anafichua udhaifu au unyonge wa mwanadamu na kutambua nguvu za Mungu, akithibitisha kwamba maisha yetu na historia ya ulimwengu huu viko mikononi mwake. Katika mstari wa mwisho (10) tunaona wazo la Uhai na roho ya kila kiumbe hai kama zawadi kutoka kwa Mungu. Hapa tunakumbushwa kuwa na tabia ya shukrani na kutegemea Mungu kwa baraka za uhai, akili, na nguvu. Kumbuka, tunafanya yote tunayofanya kwa sababu Mungu ametupa zawadi ya Uhai kwanza.
Kuna mambo kadhaa tunayoweza kujifunza kutoka kwa somo hili.
Kwanza, somo hili linatupa nguvu sisi wachungaji kuongoza kwa hekima ambayo haipatikani katika maarifa ya kibinadamu tu bali kwa kuongozwa na hekima ya Mungu inayoonyeshwa katika viumbe vyote. Linatukumbusha kuona kila tukio, kila changamoto, na kila kiumbe kama chanzo cha kujifunza kiroho, ambacho kinaweza kutusaidia kufanya maamuzi ya hekima, ya haki, na ya maendeleo kwa kanisa. Zaidi ya hayo, tunapewa changamoto ya kipekee kama wachungaji: kujumuisha viumbe vya Mungu katika mafundisho yetu, kutumia mifano kutoka kwa maisha ya kila siku, wanyama, mimea, au hata waumini, kama mwongozo wa kuelewa hekima na utaratibu wa Mungu.
Pili, somo hili linasisitiza kutegemea mamlaka ya Mungu. Wachungaji wanapofahamu kwamba hakuna kiumbe au tukio linalotokea bila idhini ya Mungu, wanapata msingi imara wa kuongoza kwa unyenyekevu na wajibu. Mamlaka ya kiroho lazima iungane na kutambua uongozi unaotunza kila uhai, kwa kuwa uhai na roho ni zawadi kutoka kwa Mungu, si mali zetu binafsi. Hii inawatia moyo sisi wachungaji kuthamini kila kiumbe na kila muumini tunapohudumu, tukitambua kwamba kila mmoja ni mwongozo wa kiroho na chanzo cha hekima ya Mungu.
Tatu, somo hili ni mwongozo wa maisha ya kiroho na kijamii. Linawatia changamoto wachungaji kuhakikisha kwamba kanisa linaendeshwa kwa hekima, wajibu, na shukrani kwa Mungu, huku likiwatunza waumini kimwili na kiroho. Wachungaji tunapofundisha kwa njia hii, tunachangia si tu katika uumbaji wa kiroho wa waumini, bali pia katika kuimarisha umoja wa kanisa na ustawi wa jamii. Kwa ujumla, somo hili linatupa mwongozo wa vitendo: kutazama asili na uhai wa kila kiumbe, kutegemea mamlaka ya Mungu, na kuthamini zawadi ya uhai, ili uongozi wetu kama wachungaji uweze kuwa na athari nzuri kwa dayosisi yetu, kanisa, na jamii kwa ujumla.
Kama tungekuwa na muda wa kujadili kidogo, ningependa kujadiliana swali hili. Kwa kuwa Ayubu anatuhamasisha kujifunza kutoka kwa wanyama, ndege na ardhi, je, tunalitazamaje somo la viumbe kama mwalimu wa hekima katika huduma yetu ya kichungaji?
Naweza kuhitimisha kwa kuwashukuru ninyi nyote mliobarikiwa kujiunga nami katika tafakuri hii. Ninashukuru sana mratibu wetu wa programu kwa kunipa fursa ya kuongoza Masomo ya Biblia leo. Mungu wa amani awe nanyi nyote. Amina (Warumi 15:33).
Mchg. Dk. Johnson Gudaga
@05/03/2026