Lupembe, Njombe

Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Dayosisi ya Kusini limeandika historia mpya baada ya kufanya ibada maalum ya ubarikio wa wachungaji wapya wanne katika Jimbo na Usharika wa Lupembe. Tukio hili la kipekee linakuwa ni la tatu pekee la ubarikio kufanyika katika usharika huo, likifuatia lile la mwaka 1934 na 1984.

Ibada hiyo ya kihistoria imeongozwa na Askofu wa KKKT Dayosisi ya Kusini, Mchungaji Dkt. George Mark Fihavango, akisaidiwa na Msaidizi wa Askofu, Mchungaji Dkt. Johnson Lunanilo Gudaga, pamoja na Wakuu wa Majimbo kutoka Dayosisi hiyo.

Wachungaji wapya waliobarikiwa na kuwekwa rasmi kwa ajili ya kuanza huduma yao katika shamba la Bwana ni:
- Mchungaji Daudi Msuya
- Mchungaji Michael Kaduma
- Mchungaji Sharon Keneth Kaduma
- Mchungaji Zakayo Ngachenga

Akihubiri katika ibada hiyo, Msaidizi wa Askofu Dkt. Gudaga amewataka wachungaji hao wapya kulitumikia Kanisa kwa uaminifu, unyenyekevu na hofu ya Mungu. Aliwasisitiza kulitanguliza Neno la Mungu katika huduma yao na kuwa watumishi waaminifu kwa watu wanaowakabidhiwa kuwachunga.

Zaidi ya hayo, upekee wa ibada hii umeongezwa kwa kufanyika ndani ya jengo la Kanisa la Usharika wa Lupembe lenye historia ya zaidi ya miaka 100. Tukio hili limeifanya siku hiyo kuwa ni muunganiko wa historia ya Kanisa la zamani na mwanzo wa kizazi kipya cha watumishi wa Injili.

Kwa namna ya pekee, wachungaji hao wanne wamekuwa sehemu ya historia hii, wakitoka katika eneo ambalo tayari limeweka alama kubwa katika safari ya Kanisa kwa zaidi ya karne moja.
Dayosisi ya Kusini inawapongeza wachungaji hao wapya kwa hatua hii muhimu, huku ikiwaombea Mungu awajalie neema, hekima, na nguvu katika kutekeleza wito wao wa kichungaji, huku wakisimamia andiko lisemalo:
”Mimi na nyumba yangu tutamtumikia BWANA.” — Yoshua 24:15



